WADAU WAELEZEA WASI WASI WA ONGEZEKO LA MAAMBUKIZI YA HIV MIONGONI MWA VIJANA POKOT MAGHARIBI.

Huenda maambukizi ya virusi vya ukimwi katika kaunti ya Pokot magharibi vikawa juu kutokana na hali kwamba wengi wa wakazi wanaougua virusi hivyo hawajitokezi kupimwa kufahamu hali yao.

Akizungumza katika bustani ya chelang’a mjini Makutano wakati wa maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, waziri wa afya kaunti ya Pokot magharibi Cleah Parklea alisema takwimu zilizopo kwa sasa kuhusu maabukizi ni za mwaka jana ambazo ziliashiria kwamba asilimia 1.6 ya wakazi wanaugua virusi hivyo.

Aidha Parklea alisema kwamba asilimia kubwa ya waathiriwa wa virusi vya HIV katika kaunti hii ni vijana.

“Kwa sasa tunaenda na takwimu zilizopo ambapo mwaka jana ilibainika kuwa ni asilimia 1.6 ya wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi wanaougua virusi vya HIV. Tatizo lililopo ni kwamba watu wetu hawaji kupimwa kufahamu hali yao na hali hii inaashiria huenda idadi ya wanaougua imeongezeka. Kulingana na takwimu zilizopo, wengi wa wanaogua virusi hivi ni vijana.” Alisema Parklea.

Mshirikishi wa huduma za HIV katika shirika la Ampath Dkt Samson Ndege alitoa wito kwa vijana hasa wanafunzi kujitenga na ngono za mapema, akiwashauri walio katika ndoa kusalia waaminifu katika ndoa zao kama njia moja ya kusalia salama dhidi ya maambukizi ya HIV.

“Tunatoa wito kwa vijana hasa wanafunzi kujitenga na ngono za kiholela na badala yake watumie muda wao mwingi kwa shughuli zao za masomo. Na wale walio kwenye ndoa wasalie waamanifu kwa wenzao na kama mtu hawezi kuwa mwaminifu basi atumie kinga iwapo ni lazima ashiriki mapenzi ili kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV.” Alisema Ndege.

Baadhi ya wanaogua virusi hivyo walielezea changamoto ambazo wanapitia kuu zaidi ikiwa unyanyapaa ambao wanatendewa na jamii.

“Tunakabiliwa na changamoto nyingi sana na mbaya zaidi ni hali ambapo hata watu waliokuwa karibu nawe hawataki tena kujihusisha nawe. Ukiuliza mtu kitu anakwambia mimi simezi dawa kama wewe sasa hali hii inatuumiza sana.” Alisema mmoja wa waathiriwa.