MWAMKO MPYA KWA ELIMU NA DINI KERIO VALLEY.
Kunashuhudiwa mwamko mpya eneo la bonde la kerio baada ya shirika la Christian impact Mission, serikali na wadau wengine pamoja na wakazi kuanza kuinua elimu na dini kwenye eneo hilo ambalo limekumbwa na utovu wa usalama kwa muda katika juhudi za kuafikia amani.
Kupitia kwa mfumo wa Biblical World view Model chini ya mpango wa kubadilisha akili na mbinu mbadala za kujikimu, shirika la CIM na serikali imekuwa ikijenga shule na makanisa kwa kusaidia watoto wenye umri wa miaka 3 hadi 4 kwenda shule.
Awali eneo hilo halikuwa na shule ama kanisa hata moja na kusalia nyuma kimaendeleo huku wakazi wakiamini kwenye mila na utamaduni potovu.
Gavana wa kaunti ya Baringo Benjamin Cheboi alielezea kujitolea kwa serikali yake kushirikiana na mashirika mbali mbali kwenye kaunti hiyo kuhakikisha kwamba uvamizi unamalizwa na amani kuafikia ili kuruhusu shughuli za maendeleo kuafikiwa na elimu kurejelewa kikamilifu.
“Serikali ya kaunti itashirikiana kikamilifu na mashirika haya lengo kuu ni kuhakikisha kwamba tunamaliza kabisa swala la uvamizi ambao umepelekea kupotea kwa maisha ya wakazi wengi ambapo hata wengine wamelazimika kuyahama makazi yao.” Alisema Cheboi.
Juhudi za mashirika hayo zimeanza kuzaa matunda ambapo baadhi ya waliokuwa wakiendeleza wizi wa mifugo wakiongozwa na Loripo Lotiko wameasi hulka hiyo na kuanza kujishughulisha na mswala mengine katika jamii.
“Tunashukuru mashirika haya kwa sasa watu ambao tulikuwa tunaendeleza uvamizi tumeokoka na tumejitenga na wizi wa mifugo. Watoto wetu sasa wanaenda shule, na sisi tunaenda kanisani.” Alisema Lotiko.
Wiki jana wadau wa maendeleo waliandaa siku ya wadau na kuzindua madarasa mapya katika shule ya msingi ya Solulu iliyojengwa na shirika la CIM Compassion International, serikali ya kaunti ya Baringo, ofisi ya mbunge, kuzinduliwa kwa shirika la vijana, kuweka ua la ujenzi wa chumba cha maakuli, kituo cha wageni na bweni ili kupanua kituo cha Komolyon eneo la Mosolion, kaunti ya Baringo.