WAZAZI WATAKIWA KUWA MAKINI NA WANAO WAKATI HUU WA LIKIZO NDEFU.


Wazazi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kuwa waangalifu na wanao hasa wakati huu ambapo wanafunzi wapo nyumbani kwa likizo ndefu ya mwezi desemba.
Ni wito wake mshirikishi wa baraza la wazee katika kaunti hii Joseph Lopetakori ambaye alisema kwamba ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha usalama wa mwanaye, na kuwahusisha katika shughuli mbali mbali zitakazowazuia kujihusisha na maswala yaliyo kinyume cha maadili.
“Kwa sasa watoto wako nyumbani kwa likizo ndefu baada ya kufungwa shule. Nawaomba wazazi wote katika kaunti hii kuwa waangalifu na wanao. Hii ni likizo ambayo kuna sherehe nyingi na iwapo watoto hawataangaliwa vizuri wanaweza kujihusisha na mambo yasiyofaa. Wazazi wanapasa kuwahusisha watoto katika shughuli mbali mbali ili wasipate nafasi ya kujihusisha na utovu wa maadili.” Alisema Lopetakori.
Aidha Lopetakori aliwataka wazazi kutotumia likizo hii kujihusisha na tamaduni iliyopitwa na wakati ya ukeketaji kwani sasa tamaduni hiyo hairuhusiwi katika jamii.
“Nawaambia wazazi wasitumie wakati huu kuwakeketa watoto. Hii tamaduni ilipitwa na wakati na hata kisheria hairuhusiwi. Tunataka likizo hii ikikamilika watoto wote warejee shuleni wakiwa katika hali nzuri.” Alisema.
Wakati uo huo Lopetakori alitoa wito kwa wakazi wa maeneo ya mipakani pa kaunti za bonde la kerio kuishi kwa amani na kujitenga na visa vya wizi wa mifugo ambavyo kwa kipindi kirefu vimekuwa chanzo cha utovu wa usalama eneo hili.
“Nawaomba wakazi wote wa kaunti hii na kaunti za bonde la kerio hasa wanaoishi maeneo ya mipakani kuishi kwa amani. Tunahitaji usalama hasa kipindi hiki cha sherehe nyingi. Wakazi wanapasa kujiepusha na tabia ya wizi wa mifugo ambao umekuwa chanzo cha utovu wa usalama eneo hili.” Alisema Lopetakori.