SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YATARAJIWA KUZINDUA ZOEZI LA KUWACHANJA MIFUGO.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin anatarajiwa kuongoza shughuli ya mwezi mmoja ya kuchanja mifugo ambayo inatarajiwa kuanza tarehe 8 mwezi Desemba.

Akizungunza na wanahabari Kachapin alisema kwamba zoezi hilo litaendelezwa katika kaunti zote ndogo za kaunti ya Pokot magharibi na baadhi ya maeneo ya taifa jirani la Uganda, magonjwa ya mapafu pamoja na miguu na midomo yakilengwa katika zoezi hilo.

“Zoezi la kuwachanja mifugo wetu litaanza tarehe 8 mwezi desemba na tunalenga kuwachanja mifugo kwenye kaunti zote ndogo kaunti hii ya pokot magharibi na baadhi ya maeneo ya Uganda. Tunataka tuhakikishe kwamba mifugo wetu wanakuwa salama dhidi ya magonjwa ya mapafu na miguu na midomo.” Alisema Kachapin.

Kachapin alitoa wito kwa wafugaji wote katika kaunti ya Pokot magharibi kutumia nafasi hiyo litakapoanza zoezi hilo ili kuhakikisha usalama wa mifugo wao ikizingatiwa ndilo tegemeo kubwa kwa uchumi wa wakazi wengi kaunti hiyo.

“Nawataka wafugaji wote kuhakikisha kwamba wanawaleta mifugo wao wapate chanjo ili kuwahakikishia afya bora kwa sababu hii ndiyo raslimali inayotegemewa na wakazi wengi wa kaunti hii kwa maswala ya kiuchumi.” Alisema.