SERIKALI YATAKIWA KUIMARISHA USALAMA WA WAFUGAJI WANAPOHAMA KUTAFUTA LISHE KWA MIFUGO.

Serikali imetakiwa kuimarisha usalama eneo la Amudat mpakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na taifa jirani la Uganda ili kutoa ulinzi kwa wafugaji wanaohamisha mifugo wao kuwatafutia lishe kufuatia ukame ambao umekithiri.

Mwakilishi wa kike eneo la Amudat Betty Rouke amesema kwamba mara nyingi wahalifu hutumia fursa hii kuwashambulia wafugaji wanaohama kutafuta lishe kwa mifugo wao na kuwaibia na hata kusababisha maafa.

“Tunakaribia kipindi cha ukame ambapo wafugaji huhama kutoka eneo moja hadi lingine kutafuta lishe kwa mifugo wao. Naomba idara ya usalama kuhakikisha usalama kwa wafugaji kwa sababu wezi hutumia fursa hii kuwashambulia na kuiba mifugo.” Alisema Rouke.

Aidha ametumia fursa hiyo kuwahimiza wafugaji wanaohamia maeneo ya mbali kuwatunza vyema mifugo wao ili wasiweze kuharibu mimea ya wakazi hasa wakati huu ambapo kunashuhudiwa uhaba wa chakula.

“Nawahimiza watu wetu kuwa wanapohama na mifugo wao hadi maeneo mengine wawe waangalifu ili wasiharibu mimea ya watu wa maeneo hayo. Hiki ni kipindi ambacho kuna ukame na kidogo kilichopo kinafaa kutunzwa vyema.” Alisema.

Wakati uo huo amewataka wazazi kutowaachia wanao shughuli ya kuwapeleka mifugo malishoni na badala yake watu wazima wahusike katika shughuli hiyo.

“Swala la kutumika watoto kuwapeleka mifugo malishoni linafaa kusitishwa mara moja. Shughui hii inapasa kutekelezwa na watu wazima ili watoto wahudhurie masomo. Pia ni hatari kwa watoto pekee kuwa malishoni ikizingatiwa ripoti za uvamizi wa wezi wa mifugo.” Alisema.