UKOSEFU WA UMEME WATAJWA CHANGAMOTO KUU ENEO LA SIGOR POKOT MAGHARIBI.


Wakazi wa eneo la Tamkal wadi ya Weiwei eneo bunge la Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia ukosefu wa nguvu za umeme licha ya kampuni ya kusambaza umeme KPLC kuweka vikingi vya umeme maeneo hayo mwaka mmoja uliopita.
Wakiongozwa na Paul Yopot wakazi hao wamelalamika kwamba wanapitia wakati mgumu kutekeleza shughuli zao za kila siku kutokana na ukosefu wa umeme, akimtaka gavana Simon Kachapin aliyezuru eneo hilo majuma mawili yaliyopita kutimiza ahadi aliyotoa kwao kuhusiana na swala hilo la umeme.
“Eneo hili huwa na tatizo kubwa la umeme na sasa ni mwaka mmoj tangu kampuni ya KPLC kuweka hivi vikingi vya umeme ila umeme wenyewe haujafika. Gavana kachapin alizuru eneo hili na kutuahidi kuwa atashughulikia swala hili sasa tunamtaka kuharakisha kutimiza ahadi hiyo.” Alisema Yopot.
Kando na swala la umeme wakazi hao wamelalamikia uhaba wa maji hasa katika soko la Sigor wakitoa wito kwa idara husika kuhakikisha kwamba soko hilo linapata maji safi ili kurahisisha shughuli zao.
“Hapa sigor tuna tatizo kubwa la maji hasa pale sokoni. Tunataka idara husika kuhakikisha kwamba tunapata maji hapa kwa sababu sasa wafanyibiashara wanahangaika kutafuta maji ya kutumia katika shughuli zao.” Alisema.