TAKWIMU ZAONYESHA ONGEZEKO LA KINA MAMA WANAOTUMIA MBINU ZA KISASA ZA UPANGAJI UZAZI POKOT MAGHARIBI.
Utafiti wa hivi punde unaashiria kuwa asilimia ya wanawake hasa walio kwenye ndoa na ambao wanatumia mbinu za kisasa za kupanga uzazi katika kaunti hii ya Pokot magharibi imeongezeka mara dufu tangu mwaka 2014.
Akitoa ripoti ya utafiti huo uliondeshwa na shirika la PMA Performance Mornitoring for Action, afisa katika shirika hilo Michael Waithaka alisema kwamba asilimia ya wanaotumia mbinu hizo imeongezeka kutoka asilimia 13 mwaka 2014 hadi asilimia 30 mwaka 2021.
“Kutokana na matokeo ya uchunguzi tuliofanya hapa pokot magharibi tumeona ongezeko kubwa la matumizi ya mbinu za kisasa za upangaji uzazi miongoni mwa kina mama. Matokeo haya yanaonyesha ongezeko la asilimia 17 kutoka mwaka 2013 hadi mwaka 2021.” Alisema Waithaka.
Kuhusu swala la dhuluma za kijinsia Waithaka alisema visa hivyo vingali vinashuhudiwa katika kaunti hii ambapo kati ya wanawake watatu mmoja huripoti dhuluma hizo.
Hata hivyo alisema kuwa wengi wa wanaodhulumiwa hawatafuti msaada na kwamba miongoni mwa wanaotafuta msaada huo wengi huutafuta kutoka kwa jamii zao ila si kwa taasisi zilizojukumika kushughulikia visa hivyo.
“Tumeona kwamba dhuluma za kijinsia zingali zinashuhudiwa kwa wingi katika kaunti hii ya Pokot magharibi. Kati ya wanawake watatu kuna mmoja anayeripoti visa hivi.” Alisema.