WAASI WA ELIMU WATATIZA USALAMA LOMUT

Asasi za usalama katika serikali, kaunti ndogo ya Pokot ya kati kaunti hii ya Pokot magharibi zimetakiwa kushughulikia tatizo la vijana kujitosa kwenye visa vya uporaji na kusababisha hali ya utovu wa usalama miongoni mwa wakazi eneo hilo.

Wakiongozwa na Lomeri Kaperur, wakazi walimtaka chifu wa eneo hilo kuchukua hatua kufuatia hali ambapo vijana wengi wameacha masomo na kuanza kuzurura katika soko la Lomut na kuleta usumbufu kwa wakazi hasa wafanyibiashara.

“kuna vijana ambao wamekataa kwenda shule huku Lomut na hao ndio wanatatiza wafanyibiashara na hata wakazi kwa kuiba mbuzi na bidhaa sokoni. Naomba vitengo vya usalama vikiongozwa na chifu kufanya upesi na kuchukua hatua kabla hali haijaharibika kabisa.” Alisema Kaperur.

Amemtaka chifu wa eneo hilo pamoja na wazee wa nyumba kumi kuitisha kikao cha haraka ili suluhu la tatizo hilo lipatikane.

“Ningetaka chifu pamoja na wazee wa nyumba kumi na kamishina wa eneo hili kuitisha kikao cha haraka hapa lomut ili tujue watoto wanaofanya uovu huu ni kina nani. Kuna mmoja anasemekana kuiba mbuzi hapa na kushirikiana na mhudumu mmoja wa pikipiki kuwasafirisha.” Alisema.

Wakati uo huo Kaperur ameitaka serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi kwa ushirikiano na kaunti jirani kutafuta suluhu ya kukomesha wizi wa mifugo, akipendekeza kuwekwa alama mifugo kutoka kaunti hizi ili kuwatofautisha kama moja ya njia za kukabili wizi.

“Ili tatizo la wizi wa mifugo likabiliwe ningependa serikali ya kaunti hii na za Baringo, Turkana na Elgeyo marakwet kuweka alama mifugo ili kuwatofautisha. Hii itafanya kupata haraka mifugo ambao wameibwa.” Alisema.