UHABA WA MAJI WAZIDI KUWA KERO CHEPTUYA
Wenyeji wa eneo la Cheptuya katika wadi ya Mnagei eneo bunge la Kapenguria katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamelalamikia uhaba wa maji baada ya serikali kusitisha kwa muda mpango wa uchimbaji maji uliokuwa ukiendelezwa kwa ushirikiano na benki ya dunia.
Wakizungumza katika soko la Cheptuya wakazi hao wakiongozwa na James Walubengo walilalamikia uhaba wa bidhaa hiyo muhimu wakisema kwamba kwa sasa wafanyibiashara wanalazimika kutumia maji chafu katika soko hilo.
Walielezea hofu kwamba huenda hali hiyo ikapelekea kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa mengine yanayotokana na uchafu.
“Kuna maji ambayo yalianza kuchimbwa hapa. Tunaomba kuharakishwa uchimbaji wa maji hayo kwa sababu kina mama wameumia sana kwa kukosa maji hayo. Wanatumia maji chafu na huenda kukazuka ugonjwa wa kipindu pindu.” Alisema Walubengo.
Aidha wakazi hao waliitaka serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi kuweka mipangilio bora katika soko la Cheptuya ili kuwe na utaratibu wa shughuli za biashara wakilalamikia kutokuwepo na utaratibu unaofaa miongoni mwa wafanyibiashara mbali mbali.
“Naiomba serikali kupangilia vizuri soko hili la Cheptuya ili kila mtu awe na sehemu yake ya kuuzia. Kuna wachuuzi ambao wanauza ng’ombe sehemu ambayo haitakikani katika soko hili. Wanafaa kuhamishwa sehemu hii na kupelekwa sehemu mwafaka.” Walisema.