POLISI WAMSAKA MWANAMME ALIYEMUUA MAMAKE KUFUATIA MZOZO WA MAHINDI TRANS NZOIA.
Polisi eneo la Kiminini katrika kaunti ya Trans nzoia wanaendeleza msako dhidi ya kijana mmoja mwenye umri wa miaka 21 kwa tuhuma za kumuua mamake Judith Nafula Konya ambaye alikuwa msimamizi wa maabara katika shule ya upili ya wasichana ya St. Josephs ambaye alikuwa amepotea tangu tarehe 18 mwezi huu kabla ya mwili wake kupatikana katika mto Kiminini.
Kulingana na kamanda wa polisi eneo la Kiminini John Onditi kulikuwepo na mvutano baina ya kijana huyo na mamake kutokana na hatua ya kijana huyo kuuza mazao ya shambani kinyume na matarajio ya mamake jambo ambalo linakisiwa kusababisha kijana huyo kuchukua hatua ya kumwua mamake na kuutupa mwile wake kwenye mto huo.
Aidha Onditi alisema mtuhumiwa alitoweka tangu siku hiyo baada ya kutekeleza kitendo hicho na hadi leo hajapatikana japo maafisa wa polisi wanaendeleza msako ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Tunamtafuta kijana huyo ambaye ni mwenye umri wa miaka 21. Mamake ana miaka 50 na alikuwa akifanya kazi ya maabara katika shue ya upili ya wasichana ya St. Josephs. Tuliupata mwili wa marehemu katika mto na sasa tunasubiri upasuaji ili tubaini jinsi marehemu alifariki.” Alisema Onditi.
Mwili wa mwendazake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya mlima Elgon ukisubiri kufanyiwa upasuaji.