JUHUDI ZA MASHIRIKA YA KIJAMII POKOT MAGHARIBI ZAPONGEZWA.

Waziri wa kilimo, mifugo na uvuvi katika kaunti hii ya Pokot magharibi Wilfred Longronyang ameyapongeza mashirika ya kijamii katika kaunti hii yakiwemo ACF na FAO kwa juhudi ambazo yanafanya kuwawezesha wakazi maeneo mbali mbali.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya mwanamke wa kijijini eneo la Kerelwe kaunti hii, Longronyang alisema ni kupitia juhudi za mashirika hayo na wahisani wengine ambapo kumeafikiwa maendeleo maeneo ya mashinani hasa kuhusu usalama wa chakula.

“Tunayashukuru mashirika haya kwa juhudi zake kwenye kaunti hii hasa kwa kina mama maeneo ya mashinani na hii ndiyo njia sahihi ya kukahakikisha usalama wa chakula.” Alisema.

Aidha Longronyang alisema kuwa serikali ya kaunti hii kupitia wizara ya kilimo inaendeleza mikakati ya kutafuta suluhu ya kudumu kwa tatizo la baa la njaa kuhakikisha kwamba kaunti hii inakuwa na chakula cha kutosha siku za usoni.

“Tutajaribu kuwafikia wakulima na kuwandaa wawe tayari wakati msimu wa mvua utakapowadia waweze kuandaa mashamba yao ili wapande mapema mimea yao. Hata serikali tutahakikisha tunawaletea mapema mbegu.” Alisema.

Baadhi ya wakazi wa eneo hilo walielezea jinsi ambavyo wamenufaika kupitia shughuli zinazoendelezwa na mashirika hayo katika maeneo ya mashinani ikiwa ni pamoja na mafunzo kuhusu jinsi ya kujiendeleza kupitia kilimo na kuwekeza.

“Tumenufaika pakubwa kwa sababu tumefunzwa kuhusu maswala ya kuwekeza, ambapo kutokana na fedha ambazo tunawekeza tunaweza kuchukua mikopo kujiendeleza kibiashara. Pia wametufadhili pakubwa na mbegu za mimea.” Walisema wakazi.