OCPD WA ALALE ASUTWA KWA MADAI YA ULAJI RUSHWA.

Wahudumu wa magari yanayohudumu katika barabara ya kacheliba wamelalamikia kuhangaishwa na OCPD wa pokot kaskazini hasa eneo la Alale ambaye wanadai kwamba anawatoza shilingi 500 kila mwezi kwa kila gari linalotumia barabara hiyo.

Wakiongozwa na Rajab Lodomo madereva hao wamedai kwamba mkuu huyo wa Polisi amefanya matozo hayo kuwa sheria na amekuwa akiyasanya magari ya wanaokiuka agizo la kutoa fedha hizo na kuwatoza faini ya juu ili kuyaachilia.

“OCPD huja kuchukua magari akisema ni lazima asanyiwe. Mwezi uliopita tulimsanyia shilingi alfu 30 kwa magari 60 kwa shilingi 500 kwa kila gari. Sasa hata mwezi haujaisha anasema tumemsahau. Sisi pia tuna majukumu na magari tunayoendesha ni ya watu anataka tufanyeje sasa?” Walilalama madereva.

Madereva hao sasa wanataka viongozi wa nchi kupitia idara ya polisi kumpa uhamisho OCPD huyo ambaye wanadai kwamba amefanya maisha yao kuwa magumu wanapotekeleza shughuli zao hasa wakati huu ambapo gharama ya masiha imezidi kupanda nchini.

“Tunamwomba rais wetu atuondolee huyu OCPD wa Alale kwa sababu ametunyanyasa hata kulipa nyumba imekuwa vigumu, tumeshindwa hata kujimudu kimaisha.” Walisema.

Hata hivyo OCPD wa eneo hilo Nathan Sanya amekanusha vikali madai hayo akisema kwamba magari hayo yalinaswa katika msako unaondeshwa dhidi ya magari yanayokiuka kanuni za barabarani katika juhudi za kukabili visa vya ajali akiapa kuwa msako huo utaendelea.

“Tumekuwa na ongezeko la ajali za barabarani ambazo zinahusisha magari na pikipiki na sasa juzi tukaamua kuwa na msako wa kuhakikisha kuwa madereva wana leseni, na la kushangaza wengine hawana leseni kwa hivyo tuna magari tumeshika na msako huo utaendelea hadi tuhakikishe kuna nidhamu barabarani.” Alisema Sanya.