SAVE MOTHERS LAJITOLEA KUPUNGUZA VIFO VYA KINA MAMA WANAPOJIFUNGUA.
Gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameelezea kujitolea kwa serikali yake kuimarisha sekta ya afya katika kaunti hii kwa lengo la kuhakikisha kuwa wakazi wanapokea huduma bora za afya.
Akizungumza wakati alipokutana na shirika la marekani la save mothers katika makazi yake rasmi gavana Kachapin amesema kuwa serikali yake itafanya iwezalo kuandaa mazingira bora kwa ajili ya shirika hilo pamoja na mshirika mengine yenye nia ya kuimarisha afya ya wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi.
Rais wa shirika hilo amesema kuwa lengo kuu la shirika hilo ni kuhakikisha vifo vya kina mama wanaojifungua pamoja na watoto vinapungua katika maeneo ambayo yanaripoti kukithiri visa hivyo, na kuhakikisha kuwa afya ya akina mama inaimarika ili wajifungue salama.
Kwa upande wake naibu gavana Robert Komole ametoa wito kwa shirika hilo kupeleka huduma zake hadi maeneo mengine kama vile kacheliba, Sigor pamoja na pokot kusini ili kuwafikia wakazi wengi zaidi.
Naye mkurugenzi wa afya katika kaunti hii Dkt Jacob Ruto amesema kuwa kaunti hii ya Pokot magharibi ni moja ya kaunti ambazo zimekuwa na idadi kubwa ya visa kina mama kuaga dunia wakijifungua ila vimepungua katika siku za hivi karibuni kutokana na juhudi za maafisa wa idara ya afya.