WAKULIMA WATAKIWA KUJISAJILI KUPOKEA MBOLEA YA BEI NAFUU POKOT MAGHARIBI.
Wakulima katika kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kutumia mbolea ya bei nafuu ambayo serikali ya Kenya kwanza ilitoa kwa ajili ya wakulima katika juhudi za kuhakikisha kwamba uzalishaji wa chakula unaimarishwa humu nchini.
Ni wito ambao umetolewa na mkurugenzi wa kilimo katika kaunti hii ya Pokot magharibi Philip Ting’aa ambaye ametumia fursa hii kuwatangazia wakulima kwamba mbolea hiyo sasa ipo katika maghala ya bodi ya mazao na kilimo NCPB mjini Makutano.
Hata hivyo Ting’aa amewataka wakulima kuhakikisha kuwa wamejisajili na wizara ya kilimo wakiwa na stakabadhi hitajika katika usajili huo kama vile nakala ya kitambulisho, nakala ya hati miliki ya ardhi miongoni mwa mahitaji mengine.
Ting’aa amesisitiza kuwa ni wakulima watakaosajiliwa tu ndio watakaopokezwa mbolea hiyo.
“Nawaelezea wakulima kwamba serikali imeleta mbolea ya bei nafuu na iko kwa maghala ya NCPB. Mkulima anafaa kujisajili kwa wizara ya kilimo kabla ya kupata mboilea hiyo.” Alisema.
Aidha Ting’aa amesema kuwa sajili hiyo ni muhimu kwani ndiyo itakayotumika katika msimu wa upanzi mwaka ujao katika kubaini idadi ya wakulima katika kaunti hii ili kubaini kiwango cha mbolea ya bei nafuu itakayoletwa kwa ajili ya wakulima.
“Ni muhimu kwa kila mkulima kujisajili kwa sababu hiyo sajili ndiyo itatumika katika msimu wa upanzi mwaka ujao kuleta mbolea. Serikali inataka kfahamu ni wakulima wangapi wako katika kaunti hii ili ijue ni mbolea kiasi gani itahitajika.” Alisema Ting’aa.