MAUAJI YA WATU 11 WAKIWEMO POLISI 8 TURKANA YAENDELEA KUKASHIFIWA.

Viongozi mbali mbali kutoka eneo la bonde la kerio wameendelea kukashifu mauaji ya watu 11 wakiwemo maafisa 8 wa usalama katika kaunti ya Turkana yaliyotekelezwa jumamosi na watu wanaoshukiwa kuwa wezi wa mifugo.

Wa hivi punde kushutumu tukio hilo ni gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin ambaye ameelezea haja ya vitengo husika kuzidisha msako dhidi ya waliotekeleza mauaji hayo ili kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza mjini Makutano wakati wa kuzindua ujenzi wa bustani ya kupumzikia wakazi, Kachapin amesema kwamba ni wakati ambapo hatua zinapasa kuchukuliwa ili kutia kikomo kwa uhalifu huo ambao umegharimu maisha ya wakazi wengi katika bonde la kerio.

Aidha Kachapin amedokeza kuhusiana na kuwepo mipango ya kuandaliwa kikao cha wadau katika sekta ya usalama katika kuweka mikakati ya kukabili hali hii ambayo amesema kuwa inaathiri pakubwa mipango ya maendeleo.

“Mimi kama gavana wa kaunti ya Pokot magharibi sijafurahia maafa ambayo yamefanyika huko Turkana ambapo maafisa wa polisi wameuliwa ,na watu ambao wametekeleza mauaji hayo wanapasa kusakwa ili kuchukuliwa hatua.” Alisema.

Kuhusiana na ujenzi wa bustani hiyo kachapin amesema kwamba lengo kuu ni kuboresha sura ya mji wa Makutano mbali na kutoa mazingira bora kwa wakazi wa kaunti hii hasa wa mji wa makutano kupata sehemu ya mapumziko katika shughuli zao mbali mbali za kila siku.

“Tumezindua ujenzi wa sehemu ambako watu watakuwa wakija kupumzikia baada ya shughuli zao kwa hivyo serikali ya kaunti inataka kuboresha mji wa Makutano na sehemu zote za kaunti hii kwani ni jukumu la serikali ya kaunti kuboresha maisha ya watu wake.” Alisema.