BARAZA AWASHUTUMU WALIMU KUTUMIA CBC KULA KUKU ZA WAZAZI.


Mbunge mwenye utata wa eneo bunge la Kimilili katika kaunti ya Bungoma Didmus Baraza amewasuta walimu katika kile amedai kutumia mtaala mpya wa elimu CBC kujinufaisha kutoka kwa wazazi.
Akizungumza katika hafla moja ya mazishi eneo la Kibingei kaunti ya Bungoma, Baraza amedai kwamba walimu wamekuwa wakitumia mfumo wa elimu wa CBC kula kuku za wazazi kwa kisingizio cha kuendeleza masomo ya mtaala huo.
“Walimu wamekula kuku mpaka imeisha kwa maboma ya watu. Hiyo CBC tunataka iondolewe kabisa,” Alisema.
Kulingana na mbunge huyo, walimu wamekuwa wakiwaagiza wanafunza kuwaleta kuku hao shuleni kwa masomo ya utendaji (practicals) ambapo wanaondoa sehemu chache na kisha kubeba sehemu iliyosalia kwa matumizi yao nyumbani.
Baraza amesema kuwa ni kutokana na sababu hii ambapo uongozi wa rais William Ruto unatafakari kuhusu kuondoa mfumo huo wa elimu.