ONGEZEKO LA BEI YA MAFUTA LAZIDISHA VILIO NCHINI.


Hisia kali zimeendelea kuibuliwa miongoni mwa wananchi kufuatia hatua ya tume ya kudhibiti kawi EPRA kutangaza ongezeko la bei ya mafuta nchini.
Wakiongozwa na meshack Yego wahudumu wa boda boda mjini Makutano katika kaunti ya Pokot magharibi wamesema kuwa hatua ya kupanda bei ya mafuta itaathiri pakubwa shughuli zao kwani wateja wengi hawakubaliani na bei mpya.
“Kupanda kwa bei ya mafuta kumetuathiri sana kwa sababu sasa wateja hawataki kulipa bei mpya tunayowaambia na sasa maisha yanaelekea kuwa magumu sana kwetu.” Alisema.
Waliendelea kwa kusema, “hatujui sasa tuatishi aje katika taifa hili la Kenya. Gharama ya maisha sasa itapanda kwa sababu vitu vingi vinategemea mafuta.”
Wametoa wito kwa rais William Ruto kuingilia kati na kuwanusuru wafanyibiashara hasa katika sekta ya uchukuzi ambayo inategemea pakubwa bidhaa hiyo.
“Rais wetu ambaye tumemchagua juzi atusaidie. Kama mafuta ya Ukraine yamekuwa vigumu kuingia Kenya basi waende katika mataifa mengine kama Libya. Tunasikia huko mafuta yana gharama ya chini kwa sababu hali ilivyo sasa si nzuri.” Walisema.
Akizungumza jumanne wiki hii baada ya kuapishwa rasmi kutwaa uongozi wa taifa, rais William Ruto alitangaza kuondoa ruzuku ya mafuta akisema kwamba inagharimu serikali fedha nyingi, hali iliyopelekea tume ya kudhibiti kawi EPRA kutangaza ongezeko la bei ya bidhaa hiyo.
Bei ya Petroli imeongezeka kwa kiwango cha KSh20.