NAIBU GAVANA WA BARINGO AAGA DUNIA
Naibu gavana wa kaunti ya Baringo Charles Kipngok amefariki dunia katika uwanja wa kimataifa wa ndege JKIA usiku wa kuamkia leo akiwa safarini kuelekea Mombasa kwa kutumia ndege ya shirika la Kenya airways.
Gavana wa Baringo Benjamin Cheboi amethibitisha kufariki kwa naibu wake.
Awali kampuni ya Kenya airways ilituma taarifa kuhusu kufariki kwa abiria japo haikuwa aimetaja jina lake.
Kampuni hiyo ilisema abiria huyo ambaye alikuwa akisafiri kutoka Nairobi hadi Mombasa alikumbwa na matatizo ya kupumua kabla ya kufariki.
Rais William Ruto ametuma risala za rambi rambi kwa ndugu, jamaa, marafiki familia na wakazi wa kaunti ya Baringo kufuatia kifo cha naibu huyo wa gavana.
Katika ujumbe wake Ruto amesema kuwa kifo cha Kipngok ni pigo kwa taifa hili akimtaja mwenda zake kuwa mchapakazi aliyesifika katika sekta mbali mbali ikiwa ni pamoja na sekta ya majani chai.
Ruto ameiombea familia yake faraja wakati huu wa majonzi.
Kipngok ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa cha wakuza majani chai KTGA aliaga dunia usiku wa kuamkia alhamisi katika uwanja wa ndege wa jomo Kenyatta JKIA alipoabiri ndege kuelekea jijini Mombasa kwa mkutano wa mgavana na manaibu wao.
Hiki ni kisa cha tatu kwa abiria kufariki dunia katika ndege ya Kenya airways katika siku za hivi karibuni.
Mapema mwezi huu abiria mwingine alifariki dunia katika ndege ya shirika hilo alipokuwa akisafiri kutoka jijini Nairobi kueleka New York marekani.
Tukio lingine lilitokea awali baada ya abiria mwingine kukumbwa na matatizo ya kiafya na kufariki dunia akielekea Nairobi kutoka jijini New York.