WAKAZI POKOT MAGHARIBI WAHIMIZWA KUENDELEA KUJITOKEZA KUPOKEA CHANJO DHIDI YA CORONA.
Serikali ya kaunti ya Pokot Magharibi kupitia wizara ya Afya, idara ya chanjo na maambukizi iliandaa warsha ya siku moja na washikadau mbali mbali kubuni njia na mikakati ya kuwarai wenyeji kujitokeza na kupokea chanjo dhidi ya Corona.
Akizungumza katika kikao hicho afisa anayesimamia chanjo katika kaunti ya Pokot magharibi Noel Aker Longronyang alikiri kwamba ugonjwa wa covid 19 ungalipo na ipo haja ya wakazi kukumbatia chanjo hiyo.
Alisema kwamba hadi kufikia sasa ni watu alfu 80 pekee ambao wamechanjwa kati ya watu alfu 280 ambayo ni asilimia 14.
“Ugonjwa wa covid 19 ugalipo katika kaunti hii ya Pokot magharibi. Na sasa tumefikia asilimia 14 ya watu waliochanjwa kati ya watu alfu 280 tunaolenga kuwachanja.” Alisema.
Alielezea kukerwa na uvumi ambao unaenezwa kuhusu chanjo hiyo hali anayosema kuwa imechangia idadi kubwa ya wakazi kutojitokeza kupokea chanjo.
“Tunachoomba kutoka kwa watu wetu ni kwamba wasikilize maafisa walio na ufahamu kuhusiana na chanjo hii na wala tusifuate uvumi ambao unatolewa na watu wasio na nia njema wanaoeneza uongo kuhusiana na chanjo hii.” Alisema Longronyang.
Amesema kuwa kwa sasa chanjo zinazopatikana katika vituo vya afya kaunti hii ni pamoja na Johnson and Johnson na Pfizer.
“Kwa sasa tuna chanjo aina ya Johnson and Johnson na Pfizer ambazo zinapatikana katika zahanati zetu zote.” Alisema.