MOSES WETANGULA ATEULIWA KUWA SPIKA WA BUNGE LA KITAIFA
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Bungoma Moses Wetangula sasa ndiye spika wa bunge la kitaifa.
Wetangula alitangazwa mshindi baada ya duru ya pili ya uchaguzi kukosa kufanyika kufuatia hatua ya Kenneth Marende kujiondoa.
Katika duru ya kwanza, Wetangula alijizolea kura 215 huku Marende akipata kura 130.
Wetangula ameapishwa rasmi kuchukua nafasi ya uspika katika bunge la 13 huku Gladys boss shollei akiwa naibu spika .
Aidha Gladys boss aliibuka mshindi wa kiti cha naibu spika kwa kupata kura miamoja tisini na nane dhidi ya alizopata mbunge wa dadaab fara maalim
Maalim alijiondoa baada ya raundi hiyo ya kwanza ambapo hakuna aliyepata theluthi mbili ya kura hivyo Gladys boss kutangazwa mshindi naibu huyo wa spika aliapishwa mwendo wa saa nne usiku wa kuamkia leo.
Tayari wetangula amekabidhiwa mikoba ya uongozi na aliyekuwa spika wa bunge la 12 Justine Muturi ambaye amempongeza Wetangula akimshauri kutekeleza majukumu yake kwa busara.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Wetangula amewapongeza wabunge wa bunge hilo la 13 kwa kumchagua akiahidi kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria.
Aidha Wetangula amempongeza mshindani wake katika kinyang’anyiri hicho Kenneth Marende ambaye alijiondoa katika duru ya pili.
Wakati uo huo Wetangula amefurahishwa na ongezeko la viongozi wa kike katika bunge la kitaifa ikilinganishwa na mabunge ya awali ambapo idadi hiyo imepanda na kufikia wanawake 82.