WAKUU WA SHULE WALALAMIKIA MAANDALIZI DUNI YA KUWAPOKEA WANAFUNZI WA SHULE ZA UPILI DARAJA YA CHINI.


Baadhi ya wakuu wa shule katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamelalamikia maandalizi duni ya kuwapokea wanafunzi wa shule za sekondari kiwango cha chini yani Junior sekondari katika mtaala mpya wa elimu CBC.
Wakiongozwa na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya St. Bakhita Grace Kakuko, wakuu hao wamelalamikia uchache wa madarasa pamoja na upungufu wa walimu kufanikisha mtaala huo licha ya waziri wa elimu Prof. George Magoha kusisitiza kuwa ujenzi wa madarasa unaelekea kukamilika.
“Tumeambiwa kwamba mwaka ujao tutawapokea wanafunzi wa Junior secondary ila tunavyoona jinsi hali ilivyo huenda sisi tusiweze kuwapokea kwa wakati unaofaa kwa kuwa hatuna madarasa ya kutosha na walimu wa kutekeleza mtaala huo wa CBC.” Alisema.
Kakuko amesema kuwa ilivyo kwa sasa hawako tayari kuwapokea wanafunzi hao akiitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa shule zote zina madarasa ya kutosha pamoja na mabweni iwapo inatarajia kufanikisha mchakato huo.
“Hatuko tayari kwa swala hili labda serikali ichukue hatua za haraka kuhakikisha kuwa tuna madarasa ya kutosha pamoja na mabweni ili wanafunzi hao watakapokuja tuwe na nafasi ya kutosha ya kuwashughulikia.” Alisema.
Wakati uo huo Kakuko amelalamikia ubovu wa barabara inayoelekea katika shule hiyo hali anayosema kuwa inaathiri shughuli zao akitaka serikali kuingilia kati ili kushughulikia hali hiyo.