RUTO AWATAJA WAPIGA KURA NA MWENYEKITI WA IEBC KUWA MASHUJAA WA UCHAGUZI.
Rais mteule William Ruto amemlimbikizia sifa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC Wafula Chebukati, idara ya mahakama na wakenya wapiga kura kuwa mashujaa wa uchaguzi wa mwaka 2022.
Akilihutubia taifa baada ya mahakama ya juu kuidhinisha ushindi wake kama rais wa tano wa jamhuri ya Kenya, Ruto amesema kuwa ni muhimu kwamba taasisi hizo zilisimama wima dhidi ya wimbi ambalo huenda lililenga kubadili maamuzi ya wakenya.
Ruto amesema kuwa atamheshimu rais anayeondoka Uhuru Kenyatta na kwamba serikali yake itampa heshima zote anazostahili kama rais mustaafu wa taifa hili.
Wakati uo huo Ruto amesema kuwa wapinzani wake si maadui na kwamba atawatambua kama watu walioshiriki kukuza demokrasia ya taifa hili.
Kwa upande wake Chebukati amepongeza uamuzi huo wa mahakama akisema kuwa uamuzi huo umerejesha hadhi ya IEBC ambayo utendakazi wake ulikuwa umetiliwa shaka baada ya madai mazito kuibuliwa.
Aidha amewapogeza wakenya kwa kudumisha amani kipindi chote cha uchaguzi.
Wakati uo huo Uhuru Kenyatta aliahidi kumkabidhi mamlaka Ruto kwa kufuata kanuni za taifa kidemokrasia.
Katika hotuba kwa taifa rais Kenyatta alisema kuwa aliapa kuheshimu uongozi unaofuata sheria na kwamba mpango wa kukabidhi mamlaka tayari unaendelea huku akiwahimiza wakenya kuheshimu taasisi za kikatiba.
Rais Kenyatta alionekana kukosoa uamuzi uliotolewa na majaji wa mahakama ya juu zaidi nchini wa kutupilia mbali maswala yaliyoibuliwa katika kesi ya kupinga ushindi wa ruto bila kuyapiga msasa akisema wakati umewadia kwa wakenya kujiuliza maswali hasa kuhusu uamuzi ambao unatolewa.
Hata hivyo rais Kenyatta bila kumtaja moja kwa moja rais mteule willima Ruto amewashukuru wakenya walioshiriki uchaguzi uliopita na kuwatakia kila la heri wakilisongesha taifa mbele.