ATHARI ZA UVAMIZI ZENDELEA KUSHUHUDIWA BARINGO.
Zaidi ya familia 100 kwenye eneo bunge la Baringo kaskazini zilizokimbia makwao kutokana na utovu wa usalama sasa zanaitaka serikali kuingilia kati ili kuwapa mahitaji ya kimsingi kama vile chakula.
Familia hizo kutoka vijiji vya Ayatya, kagir, na kosile ambazo zinaishi kwenye makambi katika eneo la Rondinin zinasema kuwa uvamizi wa mara kwa mara kutoka kwa wezi wa mifugo uliwalazimu kukimbilia usalama wao.
Kulingana na waathiriwa hao wakiongozwa na michael sesat, Evelyne Tarus na Jane Kaptum kwa sasa wanapitia hali ngumu kwani hawana chakula na pia wanakabiliwa na hatari ya kuathiriwa na magonjwa.
“Shida ambayo tuko nayo ni njaa, hali ya mvua, baridi hatuna malazi. Inaelekea miezi nane tukiwa tungali tunaishi mwituni kutokana na utovu wa usalama ambao unasababishwa na wizi wa mifugo.” Wamesema.
Aidha wamesema kuwa wengi wa watoto wamelazimika kuacha masomo yao ambapo wanahofia kwamba maisha yao yataathirika iwapo hawatarejea shuleni.
“Hata sasa tuna watoto ambao wamekaa muda mrefu bila kwenda shule, hata hawajui kuzungumza Kiswahili. Tuna shida ya chakula na hata karo ya shule hatuwezi kupata.” Wamesema.
Kwa upande wake afisa mkuu mtendaji wa shirika la new dawn of hope Joan Jemutai, akiongea baada ya kuwatembelea amewarai wahisani kujitokeza na kuwapa waathiriwa hao msaada tofauti hasaa wakati huu ambapo mvua inaendelea kushuhudiwa.
“Wengi wa wakazi hao wanaugua ugonjwa wa malaria kutokana na kuumwa na mbu. Natoa wito kwa wahisani wote na mashirika mbali mbali ya kijamii, makanisa na mashirika ya kimatibabu kujitokeza ili kuwasaidia watu hawa.” Amesema Jemutai.