MACHO YOTE YAELEKEA MAHAKAMA KUU AZIMIO UKITARAJIWA KUWASILISHA KESI YA KUPINGA MATOKEO YA URAIS.
Chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya kinatarajiwa leo kuwasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa William Ruto katika matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa jumatatu iliyopita na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi IEBC Wafula Chebukati.
Leo ikiwa siku ya mwisho kwa makataa ya kuwasilisha kesi hiyo tayari mawakili wa azimio wamekamilisha shughuli ya kuandaa ushahidi wa kuwashawishi majaji wa mahakama ya juu kutupilia mbali ushindi wa Ruto.
Akizungumza katika kanisa la Jesus teaching ministry jijini Nairobi kinara wa azimio Raila Odinga ameelezea matumaini kuwa mahakama ya juu itakumbatia ombi lao la kupinga matokeo hayo akisema ukweli kuhusu uchaguzi huo utabainika.
“Tuna imani kwamba wakenya walizungumza tarehe 9 mwezi agosti na ushindi wa wakenya hautapotea kiurahisi hivi. Tuna wahakikishia waliotuunga mkono kwamba tutasimama nanyi na hatutatikisika kamwe.” Amesema Odinga.
Naye kinara mwenza martha karua amesema kuwa wabunge wapya wanafaa kuapishwa baada ya uchaguzi uliosalia kufanyika humu nchini.
“Huu uchaguzi wa Mombasa na Kakamega ukifanyika muungano wa azimio utaibuka mshindi. Leo hii tungekuwa tunajigamba tuko na magavana 24 ila wawili bado hawajashiriki uchaguzi maeneo yao. Uchaguzi huo unaahirishwa kwa lengo la kutufanya tupoteze ngome zetu.” Amesema.
Ameongeza kwa kusema kuwa, “Tunaomba uwepo wa Mungu kwamba ngome zetu zitasalia nasi hata uchaguzi uahirishwe kwa siku ngapi.”
Kauli yake imeungwa na kinara wa wiper kalonzo musyoka ambaye amekashifu tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kwa kuahirisha uchaguzi katika maeneo nane yaliyosalia.
“Tumeshiriki uchaguzi mara nyingi katika nchi hii ila hatujawahishuhudia hali ambapo tume inayowajibika kusimamia uchaguzi mkuu inaishia kubadilisha uamuzi wa watu wengi.” Amesema.