HOSPITALI YA KACHELIBA YASUTWA KWA KUWANYANYASA WAFANYIKAZI.


Wafanyikazi katika hospitali ya Kacheliba kaunti hii ya Pokot magharibi wamelalamikia hali ngumu ya maisha ambayo wanapitia wanapoendeleza shughuli zao katika hospitali hiyo.
Wafanyikazi hao wamelalamika kulipwa fedha kidogo licha ya kazi ngumu ambayo wanafanya katika hospitali hiyo, fedha ambazo hata hivyo wamedai kuwa inachukua muda kabla ya kulipwa hali ambayo imefanya baadhi ya wafanyikazi kuondoda huduma zao katika hospitali hiyo.
“Tumefanya kazi kwa miezi nane ambayo hatukulipwa kabisa na sasa tumebaki kwa madeni mengi. Tuna mahitaji mengi na pesa zetu ni kidogo sana ambazo hazifanyi chochote.” Wamesema.
Aidha wamelaumu uongozi wa hospitali hiyo ambao wanesema kuwa unaendeleza uongozi wa kiimla ambapo wanatishiwa kuachishwa kazi kila wakati wanapojaribu kulalamikia masaibu ambayo wanakumbana nayo wakitaka uongozi mpya unaokuja kaunti hii kuhakikisha hali yao inashughulikiwa.
“Tunafanya kazi ngumu na wametufinya mshahara sana. Tuna uongozi wa kiimla kwenye hospitali hii. Tukijaribu kulalamika wanasema tutafutwa kazi na sasa tunataka serikali mpya ambayo inaingia itusaidie.” Wamesema wafanyikazi hao.
Hata hivyo msimamizi wa hospitali hiyo Solomon Tukei amekanusha madai hayo ambayo ameyataja kuwa porojo, akisema kwamba ni mwezi julai pekee ambao mishahara yao haijalipwa japo akikiri kuwa wanapokea fedha kidogo ambazo amependekeza kuangaziwa upya.
“Nakanusha matamshi haya kwa kusema kwamba hamna mtu yeyote ambaye hospitali haijawahi kumlipa. Wafanyikazi wote wa kaunti hawajalipwa mshahara wa mwezi julai. Kwa hivyo huo ni uvumi ambao haupasi kusikiliozwa na mtu yeyote.” Amesema Tukei.