MIITO YA SIASA ZA AMANI YAENDELEZWA POKOT MAGHARIBI.


Miito imeendelea kutolewa kwa wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi na taifa kwa jumla kudumisha amani hasa wakati huu wa siasa za uchaguzi mkuu wa mwezi agosti ili kuandaa mazingira bora kwa ajili ya uchaguzi huo.
Wa hivi punde kutoa wito huo ni mgombea kiti cha ugavana wa kaunti hii kupitia chama cha UDA Simon Kachapin ambaye amewataka wakazi kuwapa nafasi wanasiasa wote kutangaza sera zao na kisha kufanya uamuzi wao katika uchaguzi mkuu.
Aidha Kachapin amewataka wagombea viti mbali mbali vya kisiasa katika kaunti hii kuuza sera kwa wananchi na kutotumia vijana kuvuruga amani.
Wakati uo huo gavana huyo wa kwanza wa kaunti hii amewataka wadau wa usalama kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa hasa maeneo ya mipakani pa kaunti hii ambako kumekuwa kukishuhudiwa visa vya utovu wa usalama ili kuwapa wakazi wa maeneo hayo nafasi ya kushiriki uchaguzi wa agosti 9.
Vilevile Kachapin ameitaka tume ya uchaguzi IEBC kuweka mikakati ya kutosha ili kuandaa uchaguzi usiokuwa na tashwishi hasa maeneo ambako kuna tatizo la mtandao kwenye kaunti hii ya Pokot magharibi.