AFUENI KWA WEKENYA UNGA UKIPUNGUZWA HADI SHILINGI 100 KWA KIPINDI CHA MAJUMA MANNE YAJAYO.
Katika kipindi cha siku 28 zijazo wakenya watapata fursa ya kununua unga wa mahindi kwa bei ya chini kufuatia tangazo la wizara ya kilimo kwamba mfuko wa unga wa kilo mbili taanza kuuzwa kwa shilingi 100 kutoka 250.
Wizara ya kilimo imesema kuwa hatua hiyo imetokana na uamuzi wa serikali kutoa ruzuku ya asilimia 60 ya bei ya mfuko wa kilo mbili wa unga na hivyo kufanikisha kupungua kwa bei hiyo.
Katika mpango huo uliotiwa saini na katibu katika wizara ya kilimo Francis Owino, serikali itagharamia tofauti kati ya bei iliyopunguzwa na ile halisi na kuzilipa kampuni za kusaga unga kwa kipindi cha wiki nne zijazo.
Wakenya wa matabaka mbali mbali wamepongeza hatua hiyo ya serikali wakisema kuwa hatua hii ni afueni kubwa kwa wakenya ambao wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na kupanda gharama ya maisha hali ambayo imehusishwa na vita baina ya mataifa ya urusi na Ukraine.
Yanajiri haya huku mgombea urais wa chama cha UDA William Ruto akidai kupunguzwa kwa bei ya unga kumefanywa hivyo ili kuwahadaa wakenya kumchagua Raila Odinga kuwa rais.
Ruto ameshangazwa na jinsi serikali imekuwa ikilaumu vita vya Ukraine na Urusi ambavyo vimechangia bei ghali ya bidhaa akisema vita hivyo havipasi kuhusishwa na kupanda kwa gharama ya maisha kwani serikali imefeli katika majukumu yake.