“MLINICHEZEA KISIASA, NITAWACHEZEA KISIASA.” KAULI YAKE LONYANGAPUO KUHUSU MSAADA WA CHAKULA.
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi John Lonyangapuo amepuuzilia mbali madai ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kaunti hii kwamba anatumia msaada wa chakula uliotolewa na serikali kwa ajili ya wakazi wanaokabiliwa na makali ya njaa kaunti hii kujipigia debe kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwezi agosti.
Katika kikao na wanahabari mjini makutano Lonyangapuo amesema ndiye aliyetuma maombi kwa serikali kuu kutoa msaada huo kwa wakazi wanaokabiliwa na makali ya njaa baada ya kile alichodai wabunge katika bunge la kaunti hii kulemaza juhudi zake za kutenga bajeti ya kununua chakula.
Lonyangapuo amahakikishia wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kwamba shughui ya ugavi wa chakula hicho itaendeshwa kwa uwazi bila mapendeleo yoyote kwani mfumo wake wa kubaini wanaohitaji msaada wa chakula ni thabiti na wa kutegemewa.
Viongozi mbali mbali wa kisiasa katika kaunti hii wakiongozwa na seneta Samuel Poghisio na mwakilishi wadi maalum Elijah Kaseuseu walionya dhidi ya kutumika msaada huo wa chakula kama chambo cha kuomba kura kutoka kwa wakazi wakisema umetolewa na serikali kuu ili kuwanusuru wakazi kutokana na makali ya njaa.
Wakati uo huo Lonyangapuo amepuuzilia mbali kura za maoni zinazoonyesha kuwa mpinzani wake wa chama cha UDA Simon Kachapin amempiku kwa umaarufu kwenye kinyang’iro cha ugavana wa kaunti hii akielezea matumaini ya kuibuka mshindi mwezi agosti.