MAANDALIZI YA UCHAGUZI AGOSTI 9 YAENDELEA KUIBUA TUMBO JOTO.


Tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imetakiwa kuwa na msimamo mmoja kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwezi agosti.
Ni wito ambao umetolewa na seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ambaye aliishutumu tume hiyo kwa kutoa taarifa kinzani kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, hali anayosema kuwa inatatiza kampeni zao kwa ajili ya uchaguzi huo.
Poghisi alidai kuwepo na migawanyiko miongoni mwa maafisa wa IEBC kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo.
Aidha seneta poghisio alitetea msimamo wa muungano wa azimio la umoja one Kenya wa kutumika sajili ya wapiga kura isiyo ya dijitali sawa na ile kidijitali akisema wanajaribu kuzuia hali ambapo baadhi ya wapiga kura watakosa kupiga kura iwapo mitambo ya dijitali kukosa kusoma alama za vidole vyao pamoja na tatizo la mitandao kwenye baadhi ya maeneo.
Wakati uo huo Poghisio aliwataka wagombea nyadhifa za kisiasa katika kaunti hii ya Pokot magharibi kuendesha kampeni zao kwa njia ya amani na utulivu na kuuza sera zao kwa wananchi na kukoma kurusha cheche za maneno kwa wapinzani wao.