WAGOMBEA NYADHIFA ZA SIASA POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUDUMISHA HESHIMA.

Wito umetolewa kwa wagombea nyadhifa za uongozi katika kaunti ya Pokot magharibi kuendesha kampeni zao kwa njia ya heshima, na kutowatumia vijana kuvuruga amani kwa maslahi yao ya binafsi.

Aliyekuwa chifu wa lokesheni ya Cheptulel Julius Matala ameelezea kusikitishwa na hali kuwa baadhi ya wagombea hasa wa wadhifa wa ugavana wamekuwa wakiwatumia vijana kuwakabili wapinzani wao ikiwemo kuharibu mabango yao ya kampeni.
Wakati uo huo Matala amewataka wakazi wa kaunti hii kufanya maamuzi ya busara katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti na kutokubali kushawishiwa kifedha na wanasiasa ili kufanya maamuzi ambayo huenda watajutia baadaye.

Kumekuwepo na upinzani mkali baina wagombea wawili wa ugavana kaunti ya Pokot magharibi gavana wa sasa John Lonyangapuo anayewania kupitia chama cha KUP (Kenya Union Party) na gavana wa kwanza Simon Kachapin anayewania kwa mara ya pili kupitia chama cha UDA.
Wakazi wa Pokot magharibi sasa wana nafasi ya kufanya uamuzi kwa kuzingatia utendakazi wa wagombea wote wawili ikizingatiwa wote wamewahi kuhudumu kama gavana wa kaunti hii.