MUKENYANG AAPA KUBADILISHA DHANA KUHUSU WANASIASA.
Mwaniaji kiti cha mwakilishi kina mama katika kaunti hii ya Pokot magharibi Catherine Mukenyang amesema kuwa atazingatia uwazi katika matumizi ya fedha za umma iwapo atatwaa kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti.
Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki mapema jumatatu, Mukenyang ambaye pia ni spika wa bunge la kaunti hii alisema kuwa atahakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya afisi ya mwakilishi wa kike zinayafikia makundi yanayolengwa.
Aidha Mukenyang alisema kuwa atatumia siku za kwanza 100 baada ya kuingia afisini kuweka mikakati ya jinsi ya kushughulikia makundi mbali mbali chini ya afisi yake ikiwemo kuandaa vikao na makundi haya kuhusu maswala ambayo yanapasa kupewa kipau mbele.
Wakati uo huo mukenyang alisema analenga kubadilisha dhana ambayo imekuwepo kwamba wanasiasa ni wabinafsi, akiwahakikishia wakazi wa kaunti hii kwamba uongozi wake utazingatia uadilifu wa hali ya juu na huduma kwa mwananchi.