MWANAMMKE MMOJA ATIWA NGUVUNI KWA MADAI YA KUCHOMA MWANAWE NA MJUKUU WAKE KWA KUTUMIA KIJIKO KIMOTO KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI
Mama mmoja kutoka eneo la Kamuino kaunti hii ya Pokot magharibi anazuiliwa na maafisa wa polisi wa kituo cha Makutano baada yake kudaiwa kuwajeruhi vibaya mwanaye mmoja pamoja na mjukuu kwa kuwachoma kwa moto.
Akithibitisha hayo mwenyekiti wa mpango wa nyumba kumi katika kijiji hicho David Plimo amesema kuwa alipokea simu kutoka shuleni wanakosomea watoto hao kuhusu yaliyotukia kabla yake kufika shuleni humo na kuthibitisha unyama waliopitia watoto hao.
Amesema kuwa alilazimika kufika katika kituo cha polisi kuripoti kisa hicho ambapo kwa msaada wa maafisa wa polisi walimsaka mtuhumiwa na kumtia mbaroni ili kuwajibishwa kwa makosa ya kuwajeruhi watoto hao.
Plimo amewataka wazazi kutumia mbinu zinazokubalika kuwaadhibu wanao ambao wanahisi kwamba wamefanya makosa badala ya kutekeleza unyama kama huo.
Amezitaka idara za usalama kuhakikisha kuwa mhusika anachukuliwa hatua kali za kinidhamu ili liwe funzo kwa wazazi wengine wenye tabia kama hiyo.