VIJANA POKOT MAGHARIBI WAKASHIFU VURUGU ZINAZOSHUHUDIWA KATIKA MIKUTANO YA KISIASA.
Wananchi wa matabaka mbali mbali nchini wameendelea kukashifu vurugu ambazo zilishuhudiwa katika mkutano wa muungano wa Kenya kwanza hiyo jana katika uwanja wa Jacaranda jijini Nairobi ambapo makundi mawili pinzani yalikabiliana.
Vijana mjini makutano katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamekashifu vikali kisa hicho na kuwahimiza vijana kudumisha amani kipindi hiki na kutokubali kutumika na wanasiasa kuvuruga amani kwani ndio watakaokumbana na mkono wa sheria.
Vijana hao sasa wanaitaka serikali kupitia vitengo vya usalama kuendesha uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na kuwachukulia hatua wahusika wote ili kutia kikomo uovu huo nchini.
Wakati uo huo vijana hao wametoa wito kwa viongozi wa kisiasa nchini kutumia majukwaa yao ya kisiasa kuhubiri amani wanapoendeleza siasa zao na kutowatumia vijana kuvuruga amani kwa manufaa yao ya binafsi.