VIONGOZI WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA IDARA ZA USALAMA KUKABILI UTOVU WA USALAMA BONDE LA KERIO.
Wito umetolewa kwa viongozi wote kutoka kaunti zinazopatikana katika bonde la Kerio kushirikiana na vitengo vya usalama ili kukabili utovu wa usalama eneo hili ambao umepelekea wakazi wengi kupoteza maisha na hata wengine kulazimika kuyahama makazi yao.
Ni wito wake kamishina wa kaunti hii Apolo Okelo ambaye aidha amewasuta viongozi hao kwa kile amedai kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na badala yake kusubiri hadi yatokee maafa kabla ya wao kufika maeneo hayo.
Wakati uo huo Apolo amewataka wakazi wa maeneo haya pia kushirikiana na maafisa wa usalama kwa kutoa habari kuhusu wahalifu wanaotekeleza uovu huo ambao unachangiwa pakubwa na wizi wa mifugo.
Aidha Apolo ametoa hakikisho kwa wakazi wa kaunti hii hasa maeneo ya mipakani ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama kuwa idara yake itahakikisha visa hivi vinakabiliwa huku pia akitoa onyo kali kwa wahalifu wanaotekeleza uovu huo kuwa watakabiliwa vikali.