ONYO KALI YATOLEWA KWA WAGEMAJI WA POMBE KACHELIBA NA KONYAO KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI
Wagemaji wa pombe haramu eneo la Kacheliba katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameonywa vikali dhidi ya biashara hiyo kufuatia lalama za wakazi kuhusu kukithiri kwa biashara hiyo eneo hilo hasa eneoi la Konyao.
Ni onyo ambalo limetolewa na kamanda wa Polisi eneo hilo Victor Nzaka ambaye amemwagiza OCS wa eneo hilo kuhakikisha kwamba biashara hiyo inakabiliwa vilivyo, akiahidi kuimarisha msako dhidi ya wagemaji hao kwa kuongeza maafisa zaidi wa kuwakamata wahusika.
Aidha Nzaka amesema kuwa oparesheni hiyo itandelezwa hadi kwenye baa akisema kuwa vijana wengi wamekosa nidhamu na hata wengine kuacha masomo kutokana na kukithiri kwa biashara ya vileo eneo la Konyao.
Amri hiyo ya kamanda wa polisi imetokana na malalamishi ya wakazi wa eneo hilo ambao wamesema kuwa biashara ya pombe haramu imekithiri eneo hilo hali ambayo imeathiri pakubwa wakazi wakitaka serikali kuingilia kati kuhakikisha kwamba inakabiliwa.