GHARAMA YA MAISHA YAATHIRI ZOEZI LA KUWASAJILI WANAFUNZI KATIKA KIDATO CHA KWANZA.
Gharama ya juu ya maisha imepelekea kusita zaidi zoezi la kuwasajili wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza.
Haya ni kwa mujibu wa baadhi ya wakuu wa shule katika kaunti hii ya Pokot magharibi ambao wamesema kuwa idadi ya wanafunzi ambao wamejiunga na shule zao ni ya chini mno ikilinganishwa na idadi ambayo shule hizo zilitengewa.
Wakiongozwa na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Holy Cross Kacheliba Stanley Pilakan, wakuu hao sasa wanatoa wito kwa wazazi ambao wangali na wanao nyumbani kufanya hima na kuwapeleka shuleni hasa ikizingatiwa muhula huu ni mfupi mno.
Wakati uo huo Pilakan amelalamikia kiwango cha fedha ambacho serikali imetuma kwa shule nchini akisema kuwa ni cha chini mno ikizingatiwa mahitaji ya shule za upili ambapo wamelazimika kuwahudumia wanafunzi ambao wanafika bila karo kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.