UTOVU WA USALAMA WAENDELEA KUSHUHUDIWA MIPAKANI PA POKOT MAGHARIBI NA ELGEYO MARAKWET.

Viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kushutumu uvamizi ambao unaendelea kushuhudiwa mipakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet.
Wakiongozwa na seneta wa kaunti hii Samwel Poghisio, viongozi hao wamesema kuwa watu wengi wameuliwa kufuatia uvamizi huo huku wengine wakiachwa na majeraha mabaya, akiongeza kuwa ni kutokana na hali hii ambapo maeneo hayo yamesalia nyuma kwa maswala ya maendeleo.
Poghisio amewataka wakazi wa maeneo haya kusitisha visa hivi na kuishi kwa amani huku pia akitoa wito kwa viongozi kutoka pande zote mbili kuandaa vikao vya kutafuta suluhu la kudumu kwa visa hivi ili maeneo haya pia yakaweze kunufaika na miradi ya maendeleo.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na mgombea kiti cha ubunge eneo bunge la Kapenguria Nicholas Siwatum ambaye ametaja ardhi kuwa chanzo cha uvamizi huo akitaka idara za usalama kufanya juhudi kuhakikisha kuwa visa hivi vinakomeshwa.