MKUTANO WA CHAMA CHA KANU WAHAIRISHWA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI


Chama cha KANU kimetangaza kuahirisha mkutano wa chama hicho uliokuwa umeratibiwa kuandaliwa kesho ijumaa katika kaunti hii ya Pokot magharibi hadi siku ambayo itatangazwa baadaye baada ya kusuluhishwa tatizo la uhaba wa mafuta nchini.
Akitangaza hatua hiyo naibu gavana kaunti hii Nicholas Atudonyang ambaye ametangaza nia ya kuwani kiti cha ugavana kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi agosti amesema wameafikia hatua hiyo kutokana na idadi kubwa ya wafuasi wa chama hicho wanaonuia kuhudhuria mkutano huo ila wanakabiliwa na changamoto ya usafiri kutokana na gharama ya usafiri ambayo imesababishwa na uhaba wa mafuta.
Wakati uo huo Atudonyang ametumia fursa hiyo kukanusha madai kuwa chama cha KANU hakina umaarufu tena katika kaunti hii ya Pokot magharibi akitoa hakikisho la chama hicho kupata uungwaji mkono mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Amesema kuwa atahakikisha wakazi wa kaunti hii wananufaika na raslimali zinazotengewa serikali za kaunti kwa kuhakikisha kuwa swala la ufisadi linakabiliwa kikamilifu iwapo atachaguliwa kuwa gavana wa kaunti hii.