EACC YASHINIKIZWA KUHARAKISHA UCHUNGUZI WA MATUMIZI YA FEDHA POKOT MAGHARIBI.
Aliyekuwa gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameendelea kuwahimiza wakazi wa kaunti hii kumuunga mkono kuwania tena kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao ili kukamilisha miradi ya maendeleo aliyoanzisha katika muhula wake wa kwanza wa uongozi.
Kachapin ambaye pia alikuwa katibu katika wizara ya michezo tamaduni na toradhi za kitaifa kabla ya kujiuzulu ili kuwania tena kiti cha ugavana wa kaunti hii amedai kuwa gavana wa sasa John Lonyangapuo aliitenga miradi iliyoanzishwa naye na sasa analenga kuikamilisha iwapo atachaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Aidha kachapin ameendeleza shutuma zake kwa serikali ya gavana Lonyangapuo akidai imehusika pakubwa katika uporaji wa mali ya umma huku akiisuta tume ya maadili na kukabili ufisadi EACC kwa kuchukua muda kumchunguza gavana Lonyangapuo licha ya visa hivyo kuwa wazi.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na mbunge wa kapenguria Samwel Moroto ambaye aidha amedai kuwa tume hiyo inatekeleza majukumu yake kwa miegemeo ya kisiasa ambapo wanaoandamwa zaidi kuhusu maswala ya ufisadi ni viongozi wanaoegemea mrengo wa naibu rais William Ruto.