UTOVU WA USALAMA WAENDELEA KUSHUHUDIWA MARAKWET MAGHARIBI.


Viongozi katika kaunti ya elgeyo marakwet wameshutumu mauaji ya watu wawili yaliyotekelezwa na wezi wa mifugo katika eneo la koitilial, eneo bunge la marakwet magharibi hapo jana.
Wakiongozwa na naibu gavana Wesley Rotich na mwaniaji wadhifa wa ubunge eneo la marakwet magharibi wakili Timothy Toroitich viongozi hao wameisuta serikali kwa madai ya kufumbia macho swala la utovu wa usalama katika bonde la kerio wakati ambapo wakazi wanaendelea kuuliwa kila wakati na wengine kutoroka makwao kutokana uvamizi unaotekelezwa na majangili wachache.
Viongozi hao wameitaka serikali kuhakikisha kwamba usalama unarejea katika eneo hilo huku wakisema, huenda wakalazimika kuwasaidia wakazi kutafuta mbinu za kujilinda wenyewe kwani serikali imewatelekeza na kupuuza kilio chao.
Watu wawili waliojeruhiwa wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya moi mjini eldoret katika kaunti ya uasin gishu huku watano wakiwa wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya iten.