SPIKA AKANA KUWEPO MIPANGO YA KUWAZUIA BAADHI YA WABUNGE KUHUDHURIA VIKAO POKOT MAGHARIBI.
Vikao vya bunge la kaunti hii ya Pokot magharibi vikitarajiwa kurejelewa hii leo spika wa bunge hilo Catherine Mukenyang amepinga madai ya kuwepo mipango ya kuwazuilia baadhi ya wabunge kuhudhuria vikao hivyo.
Mukenyang ambaye anatarajiwa kuongoza vikao vya leo baada ya kurejea afisini kufuatia maagizo ya mahakama yaliyositisha kwa muda kubanduliwa kwake, amewahakikishia wabunge katika bunge hilo kuwa hamna atakayezuiliwa akiyataja madai hayo kuwa propaganda zisizo na msingi.
Aidha Mukenyang ametetea hatua yake kurejelea shughuli zake bungeni akisema kuwa yuko kazini kulingana na sheria hasa baada ya kupata maagizo ya mahakama, akisema kuwa hatua ya kuzuiliwa awali kuingia bungeni ilikuwa tofauti za kisiasa tu ambazo hata hivyo zilisuluhishwa.
Kuhusu swala la kukarabatiwa bajeti ya bunge hilo Mukenyanga amewataka wakazi wa kaunti hii kuwa na subira wakati mdhibiti wa bajeti akishughulikia swala hilo huku akijitetea kuwa bajeti hiyo ilipitishwa wakati ambapo hakuwa amerejelea majukumu yake.