MIKAKATI YAENDELEA KUWEKWA KUKABILI MABADILIKO YA HALI YA ANGA TRANS NZOIA.


Shirika la climate change Governance chini ya mradi wa Anglican Development Services kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Trans Nzoia zimebuni mfumo utakaowezesha Kaunti ya Trans Nzoia kupata ufadhili wa kifedha ili kushughulikia maswala ya mabadiliko ya hali ya anga.
Kwa mujibu wa Brenda Akinyi Okongo mshirikishi wa mradi huo nyingi za serikali za Kaunti zimekosa kufaidi ufadhili wa fedha za kukabili mabadiliko hayo kutokana na ukosefu wa sheria na mfumo mwafaka ambayo ni baadhi ya vigezo vya kufaidi fedha hizo, akiongeza kuwa ushirikiano wa kubuniwa kwa mfumo na sheria hizo utatoa nafasi kwa serikali ya Kaunti ya Trans Nzoia kupata ufadhili huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa wizara ya Mazingira Kaunti ya Trans Nzoia Godfrey Wekesa amesema kuwa mbali na kuvutia ufadhili wa kifedha kukabili mabadiliko ya hali ya anga, kubuniwa kwa mfumo na sheria hiyo pia kunatoa nafasi ya kushirikisha umma katika viwango vya wadi na vijiji kutekeleza miradi ya kukabili mabadiliko ya hali ya anga maeneo ya mashinani.