BUNGE LA SENETI KUANZA MJADALA KUHUSU SHERIA ZA VYAMA VYA UCHAGUZI.
Bunge la seneti linatarajiwa kuanza leo vikao vyake vya kujadili mswada wa mabadiliko ya sheria za vyama vya kisiasa ambao ulijadiliwa na kupitishwa wiki iliyopita na bunge la kitaifa katika vikao vilivyogubikwa na vurugu huku baadhi yao wakijeruhiwa.
Kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Samwel Poghisio amesema kuwa vikao vya leo vitahusu tu kusomwa mswada huo kwa mara ya kwanza na kisha kuelekezwa kwa kamati ya seneti ya sheria ambayo itahusisha umma kabla ya kuwasilisha ripoti bungeni ili kujadiliwa mswada wenyewe.
Poghiso ambaye pia ni seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi amewahakikishia wakenya kuwa vikao vya bunge la seneti vitaandaliwa katika mazingira yanayofaa kinyume na ilivyoshuhudiwa katika bunge la kitaifa japo akielezea matarajio ya kuwepo mjadala mkali wakati wa vikao hivyo.
Mswada huo ulipitishwa katika bunge la kitaifa baada ya kuangushwa mapendekezo yote ambayo yaliwasilishwa na wandani wa naibu rais William Ruto waliyotaka kufanyiwa marekebisho kadhaa kabla ya kupitishwa kwake hali iliyotajwa kuwa mbinu ya kuchelewesha kupitishwa mswada huo.