WAKUU WA SHULE WATETEA HATUA YA KUWAREJESHA NYUMBANI WANAFUNZI.


Baadhi ya wakuu wa shule katika kaunti hii ya Pokot magharibi wametetea hatua yao ya kuwatuma nyumbani wanafunzi kutafuta karo siku chache tu baada ya shule kufunguliwa kwa muhula wa tatu licha ya agizo la waziri wa elimu Prof George magoha la kuwataka walimu kuelewana na wazazi kuhusu jinsi ya kushughulikia swala hilo.
Akizungumza baada ya kuwarejesha nyumbani baadhi ya wanafunzi, mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wavulana ya Chewoyet Samwel Kiminisi Barasa amesema kuwa amechukua hatua hiyo kutokana na hali kuwa muhula huu ni mfupi kufuatia mitihani ya kitaifa, na itakuwa bora iwapo wanafunzi watalipa karo mapema ili kusiwe na kuhitilafiana na masomo yao.
Barasa ametoa wito kwa wazazi kushirikiana na uongozi wa shule na kutekeleza majukumu yao ya ulipaji karo kwa wakati ili kuruhusu shughuli kuendelea shuleni japo akisema kuwa uongozi wa shule hiyo upo tayari kuwasikiliza wale ambao wanataka ufafanuzi zaidi.
Wakati uo huo Barasa ameunga mkono hatua ya serikali kutaka wanafunzi kupimwa kubaini wanaotumia mihadarati na vileo kufuatia ongezeko la utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi ili kuhakikisha usalama wa majengo ya shule pamoja na wanafunzi wengine.