USAJILI WA MAKURUTU WA KDF WAINGIA LEO SIKU YA PILI.

Na Benson Aswani
Usajili wa makurutu wa jeshi la Kenya KDF umeingia leo siku ya pili vijana waliotimiza mahitaji katika kaunti 21 wakidaiwa kujitokeza katika vituo mbali mbali ili kutathminiwa.
Kulingana na msimamizi wa shughuli hiyo katika kaunti hii ya Pokot magharibi Canon Ndar shughuli hiyo imeanza vyema katika siku ya kwanza hiyo jana huku idadi ya waliojitokeza katika uwanja wa makutano ikiwa ya kuridhisha.
Amewahakikishia wote wanaoshiriki zoezi hilo katika maeneo yote ya kaunti hii ambako litaendelezwa kuwa litakuwa huru na haki ili mwisho wa siku kila mmoja aondoke akiwa ameridhika.
Shughuli hiyo inawalenga walio kati ya umri wa miaka 18 na miaka 26 kwa maafisa wa kawaida wa jeshi na hadi 30 kwa wanaolenga huduma za kiufundi, na hadi miaka 39 kwa viongozi wa dini na madaktari.
Aidha kuna fursa kwa waliokuwa katika KDF awali ambao wanaweza kuteuliwa kuwa constables wakiwa na umri wa kati ya miaka 30 na 55 na waliokuwa katika shirika la NYS wakiwa katika umri wa kati ya miaka 35 na 45.