WADAU WA ELIMU POKOT MAGHARIBI WAKASHIFU VISA VYA KUTEKETEZWA MAJENGO YA SHULE.

Na Benson Aswani
Wadau katika sekta ya elimu katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamelaani vikali utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi kufuatia visa vya kuteketezwa majengo ya shule ambavyo vimeendelea kuripotiwa nchini.
Wa hivi punde kuzungumzia visa hili ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Nasokol Cecilia Ngige ambaye amesema visa hivi ni mzigo mkubwa kwa wazazi hasa ikizingatiwa waziri wa elimu Prof. George magoha amesema kuwa ni wazazi watakaogharamia uharibifu unaosababishwa na wanafunzi.
Aidha Ngige ametoa wito kwa wazazi kutowatelekeza wanao na badala yake kuwa mfano bora kwao na kuwalea kulingana na maadili bora ya jamii ili kuepuka visa kama hivi akisisitiza kuwa nidhamu miongoni mwa wanafunzi inafaa kuanzia nyumbani.
Wakati uo huo Ngige amewataka walimu kufuatilia mienendo ya wanafunzi na kuwasikiliza iwapo wanakabiliwa na changamoto zozote kimaisha na pia kuzingatia pakubwa swala la ushauri nasaha kwa wanafunzi shuleni.