SERIKALI YATAKIWA KUSAMBAZA CHAKULA KATIKA SHULE KAUNTI YA BARINGO.
Na Benson Aswani
Kaunti ya Baringo ikiwa miongoni mwa kaunti 23 nchini zilizoathirika na ukame, baadhi ya viongozi kwenye kaunti hiyo sasa wanaitaka serikali kusambaza chakula shuleni kama njia ya kuhakikisha wanafunzi wanaendelea na masomo yao.
Kulingana na viongozi hao shule nyingi zilizoathirika zaidi kutokana na kiangazi ni zinazopatikana kwenye maeneo bunge ya Tiaty, Baringo kaskazini, Baringo kusini na baadhi ya maeneo bunge ya mogotio.
Mwakilishi wadi ya Bartabwa na ambaye ni kiranja wa wengi kwenye bunge la kaunti ya Baringo Reuben Chepsongol ameitaka serikali kuchukua hatua za haraka na kuanza usambazaji huo wa chakula.
Kwa upande wake msomi Geofrey Kiptoo anasema kuwa shughuli za masomo kwenye shule nyingi zitatatizika iwapo usambazaji wa chakula hautaharakishwa kwani maeneo bunge hayo yameathirika zaidi kutokana na kiangazi.
Hata hivyo naibu kaunti kamishna eneo bunge la Baringo kaskazini Obwocha Bobwocha amethibitisha kwamba tayari serikali inaendeleza shughuli ya usambazaji wa chakula kwenye baadhi ya shule katika eneo bunge hilo.