VIONGOZI WASHINIKIZA KUPEWA MARUPURUPU YA KUSTAAFU WALIOKUWA MADIWANI NA WABUNGE WA ZAMANI.
Ipo haja ya waliokuwa madiwani pamoja na wabunge wa zamani kupewa marupurupu ya kustaafu.
Haya ni kulingana na mbunge wa kapenguria kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Moroto ambaye amesema kuwa viongozi hao wa zamani walitoa huduma yao kwa taifa na wanastahili pia kuangaliwa jinsi inavyofanywa kwa watumishi wengine wa umma.
Moroto amesema kuwa bunge la taifa lilipasisha mswada kuhusu fedha za viongozi hao ila rais Uhuru Kenyatta akadinda kuidhinisha malipo hayo kutokana na kile amedai huenda kulikuwa na marekebisho yaliyofaa kutekelezwa kabla ya kuidhinishwa akitaka mchakato huo kuharakishwa ili walengwa wanufaike.
Viongozi hao wamekuwa wakishinikiza serikali kuwalipa marupurupu ya kustaafu kutokana na kile wanasema wanapitia hali ngumu ya maisha licha ya kutoa huduma kwa taifa.