VIONGOZI WATAKIWA KUTOTUMIA MIRADI YA SERIKALI KUJITAFUTIA UMAARUFU.
Baadhi ya viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameshutumiwa vikali kwa kutumia miradi mbali mbali kujitafutia umaarufu pamoja na kujipigia debe miongoni mwa wakazi mbele ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Seneta wa kaunti hii ya pokot magharibi Samwel Poghisio amesema kuwa baadhi ya miradi ikiwemo ujenzi wa barabara inatekelezwa na serikali kuu ila si serikali za kaunti wala mbunge hivyo viongozi kaunti hii hawapasi kuwahadaa wakazi kuwa ndio wanaoitekeleza.
Wakati uo huo Poghisio amewataka viongozi kaunti hii hasa wabunge kuheshimu uongozi wa wenzao wa maeneo mengine na kutozindua miradi ya maendeleo katika maeneo yasiyo ya utawala wao bila kuwahusisha viongozi wa maeneo hayo.
Kauli yake Poghisio inafuatia hatua ya mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto kulalamikia vikali hatua ya mbunge wa pokot kusini David Pkosing kuzindua mradi wa barabara eneo bunge la Kapenguria bila ya ufahamu wake.