ASKARI WA KAUNTI WALAUMIWA KWA KUWADHULUMU WAHUDUMU WA BODA BODA.


Askari wa kaunti mjini makutano kaunti hii ya pokot magharibi wameshutumiwa kutumia nafasi yao kuwadhulumu wahudumu wa boda boda mjini humo.
Hii ni baada ya mhudumu mmoja wa boda boda kudaiwa kuhangaishwa na mmoja wa askari hao kwa madai ya kutolipa ushuru.
Mhudumu huyo amedai kudhulumiwa na askari huyo akitaka kubadilishwa mbinu za maafisa hao za kutekeleza majukumu yao ya kukusanya ushuru kutoka kwa wahudumu wa boda boda.
Ni hatua ambayo pia imekashifiwa vikali na mwakilishi wadi maluum Elijah Kasheusheu ambaye amedai wengi wa maafisa hao wamechaguliwa kwa misingi ya kisiasa na hawajapokea mafunzo kuhusu jinsi ya kutekeleza majukumu yao.
Kasheusheu sasa anataka waziri wa biashara na viwanda katika kaunti hii ya pokot magharibi na mkurugenzi wa idara ya ukusanyaji ushuru kuweka mikakati ya kulainisha idara hiyo ikiwemo kuwafunza kuhusu sheria zinazohusu ukusanyaji ushuru ili kuepuka kuhangaishwa wananchi.